MOYO WA MSAMAHA
NA;MWINJILISTI PROCESIUS P
0755722778
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi
Sasa ni mwaka wa kumi moja majirani wawili hawaongei wala hawasalimiani kwa sababu ya ugomvi usioisha ambao chanzo chake ni “mpaka wa ardhi tangu kipindi hicho walipokuwa wanajenga ” Ingawa wanaishi kwenye eneo moja yaani ni hatua chache kutoka nyumba moja hadi nyumba ya pili lakini hawapatani kabisa. Na tatizo kubwa ni kwamba hawajapona mioyo,wamekosa moyo wa msamaha,na kusababisha uchungu na visasi vya mara kwa mara hata kupelekea watoto kushindwa kucheza pamoja! Je ndivyo Mungu apendavyo hivyo? Fikiria,Je mmoja akipata shida atasaidiwa na huyo jirani yake? Najaribu kukutazamisha taswira fulani tunazoishi nazo huku mitaani.
Sasa,nayakumbuka maneno ya busara yaliyotolewa na wazee wangu wakati ule nilipokuwa naanza kujijengea mji wangu,wazee waliniambiajirani yako ni ndugu yako,ujitahidi kuishi vizuri na majirani yako” hayo yalikuwa ni maneno ya wazee wenye busara. Nikatamani kila mmoja ajifunze kuishi vizuri na majirani zake kama nilivyofunzwa miye,mimi sijui wewe umefundishwa nini? Kama mtoto wa Mungu ni lazima ujifunze kuwa na moyo wa msamaha na waliokukosea wote na kuwapenda hasa ndugu yako aliyekuzunguka pasipo kujali imani yake,kumbuka lile neno lisemalo “asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona,hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” 1 Yohana 4:20
Leo nataka Bwana akuguse katika hili,ili moyo wa msamaha ujengeke kwako. Kumbuka “kipimo cha kusamehewa wewe kipo kwa kuwasamehe waliokukosa” hii ikiwa na maana kwamba utasamehewa kwa kadri unavyosamehe wengine ( Mathayo 6:14-15, Luka 6:38). Moyo wa msamaha ni moja ya tabia ya Mungu wetu,maana Mungu amekusamehe mangapi mpaka sasa? Kama angehesabu maovu ni nani angesimama?(Zab.130:3) Ikiwa ndivyo basi kwa nini wewe huwezi kumsamehe huyo? Kumbuka jinsi ulivyosamehewa wewe,yafaa na wewe kumsamehe aliyekukosa katika Jina la Yesu Kristo. 
Siku moja,mwanaume mmoja alisikia sikia habari ya mkewe “kwamba hajatulia kwenye ndoa yake” na kadri alipokuwa akiyasikia hayo maneno yalimuumiza hata akaamua kufuatilizia kujua ukweli wenyewe. Alipoanza kufuatilizia kwanza alichukua simu ya mkewe kuikagua( kumbuka hao wote ni wapendwa,wameokoka) akaziona kweli meseji,sauti pamoja na picha za kimapenzi na mwanaume mwingine kama alivyokuwa akiambiwa. Basi alichokifanya ni kumfukuza mkewe,ingawa ilikuwa ni kweli hayo yote na mkewe akaomba msamaha mkubwa ambao tangu azaliwe huyo mwanamke hakuwai kuomba msamaha mkubwa kama huo. Lakini haikufua dafu,bali jamaa akamfukuzia mbali,alikataa kumsamehe na kwa sababu alikuwa ameokoka akaenda kujitafutia uhalali wa kimaandiko ili amkimfukuza aseme “kama ilivyoandikwa hapa”
Hivyo akatafuta lile andiko kwenye biblia,ili akamilishe mpango wake;,akalishikilia andiko Mathayo 19:9 “ Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini. “…. Na ujue andiko hili haliruhusu kuachana kinyume kabisa na tafsiri ya wengi wenye kuelewa ndivyo sivyo!!! Hakuna mahali popote kwenye biblia panapo ruhusu kuachana kwa wanandoa.
Sasa,huyu mwanaume akamfukuza mkewe kwa sababu aliona aliona kwenye simu tu mambo ya kukosa uaminifu,kumbuka ni kwenye simu tu,jamaa akamuacha mkewe ingawa aliombwa msamaha sana. Sasa ebu leo hii jiulize kama ungelikuwa wewe ndio mwana ndoa kama huyu mwanaume,Je utamwacha mwenzako kwa kosa hili tena kwa kuona juu juu? Je wewe njia zako ziko sawa? Je ikiwa umeombwa msamaha mkubwa hivyo,kwa nini huwezi kumsamehe mwenzako ikiwa wewe mambo yako ni machafu kuliko hayo ya mwenzako? Au je unafikiri Mungu hakuoni katika mambo yako? Ikiwa utashindwa kumsamehe mwenzi wako kwa kosa lolote Je na wewe utasamehewa na Mungu makosa yako? Au je hukumu kubwa namna hiyo unayomuhukumu mwenzako,Na wewe ulipodondoka dhambini mbona hukuukumiwa? Ebu jioji,kisha chukua hatua ya kumsamehe mwenzi wako,au ndugu yako.
Hivi ni kweli kabisa wewe ni mtakatifu usiyekosea? Hivi ni kweli kabisa unafikia hatua ya kuhukumu namna hiyo? Mimi sijui,mimi ni mwanadamu tu kama wewe na kazi yangu ni kukuandikia haya,lakini ujue yupo Mungu aonaye sirini,angalia asemavyo Bwana“Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema BWANA.” Yeremia 23:24. Ifike wakati sasa uwe na moyo wa kusamehe na kuona kana kwamba hajakukosea. Wewe ni mtu wa nuru,jaribu kushuka na kumsamehe maana jiangalie na wewe pia.Mara nyingi tunapenda kuhukumu bila kuangalia makosa yetu. Na ukumbuke Mungu hadhiakiwi,chochote utakachopanda ndicho utakachovuna (Wagalatia 6:7)
Usiwe kama yule bwana aliyesamehewa deni kubwa na bwana wake,deni la talanta elfu kumi alafu akatoka na kwenda kwa mjoli wake aliyekuwa akimdai deni dogo sana,dinari mia kisha akamkaba koo mjoli wake na kumtupa gerezani,bila kuangalia kwamba yeye mwenyewe amesamehewa kiasi kikubwa cha pesa yaani kama milioni 50, lakini yeye hakuweza kumsamehe mwingine mwenye deni dogo la kiasi cha 7,500/=tu. (Mathayo 18:23-35). Ni vyema ufikiri makosa yako kisha uone vile Mungu alivyokusamehe kisha umsamehe na huyo aliyekukosa. Wala usitoe adhabu yoyote maana si kazi yako,kisasi ni kazi ya Bwana ( Warumi 12:19) Kwa sababu ukilipa kisasi ni kana kwamba unataka kuifanya kazi ya Mungu. Kazi yako ni kumsamehe na kuzidi kumuombea ageuke kutoka kwenye hayo makosa!
“ Moyo wa msamaha” ni nini haswa?
Neno “msamaha” lina maana ya kumuachilia mtu aliyekukosa kutoka moyoni na kumuona kana kwamba hajakukosea. Ni neno dogo sana lenye herufi saba tu,lakini ndilo neno pekee lenye matokeo makubwa hata kuokoa maisha ya watu. Si rahisi kuwa na moyo wa msamaha nje ya Roho mtakatifu. Ebu angalia wale wanaokosana,ni nani kati yao atakayekubali kushuka na kusema “nisamehe ” ikiwa Roho mtakatifu hakumuongoza kwa kumpa unyenyekevu wa kushuka? Hivyo utagundua unamuhitaji sana Roho mtakatifu akusaidie kukuvika moyo huu kama vazi. 
Hivyo ninapozungumzia “moyo wa msamaha“ninazungumzia tabia ya ndani ya Mungu mwenyewe aliyekusamehe dhambi zako na makosa yako pale golgota,msalabani akitarajia tabia hii ya Roho iumbike ndani yako ili na uweze kusamehe waliokukosa kwa sababu ndio kupona kwako kwenyewe. Kitendo cha kumuachilia aliyekukosa ni kumsamehe,ikiwa mtu amekukosa gafla hasira huja ndani yako, na hapo ndio kumshikilia mtu kunakoanzia. Lakini neno linatutaka uchungu,hasira na matukano yote yaondoke ndani mwetu ( Waefeso 4:31-32).Ukifanikiwa kuwa na moyo huu wa msamaha,basi ujue thamani ya wokovu wako itaonekana na hakika watu watasema umeokoka kweli kweli! 
Mambo yafuatayo hayana budi kukujia;
  1. Kukwazwa – Makwazo hayana budi kuja,lakini ole ni kwake akwazaye ( Luka17:1-4). Hata kama utakuwa mtakatifu wa namna gani,lakini ni lazima utakwazwa tu,kazi yako ni kusamehe akukwazaye na kumuombea.
  2. Aliyekukosa kutokuja kwako na kuomba msamaha – kuna wakati mwingine mtu anakukosea alafu wala hana time na wewe kukuomba msamaha,ukimsamehe sawa,usipomsamehe yeye ni saa,utajua wewe na Mungu wako!!! Lakini katika mazingira haya,wewe ni lazima umsamehe hata kama hajaja kuomba msamaha.
Je ufanye nini hata kuwa na moyo huu wa msamaha?
01. Muombe Roho mtakatifu akusaidie kukuondolea uchungu.
Kusamehe sio jambo la kitoto!!! Ni kubwa na linaumiza moyo sana. Wengi leo hawawezi kusamehe kwa sababu wakifikiri vile walivyokoswa alafu gafla wanaanza kusikia uchungu ndani yao. Na mbaya zaidi ni pale mkosa wako asiyejali kuja kwako kukuomba msamaha!!!! Sasa ki kawaida ya mwanadamu,hawezi kusamehe hata ingelikuwa kosa dogo kiasi gani bila kuwezeshwa na Mungu kwa Roho wake wa milele. Ngoja nikuoneshe hili,Petro alikuwa ni mwanafunzi wa Yesu kama ulivyo wewe leo,lakini aliumizwa na wakosaji waliokuwa wakimkosa mara kwa mara hatimaye akamfuata Yesu na kumuuliza “ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?” ( Mathayo 18:21-22). 
Hii inaonesha kulikuwa na watu wanaomkosa mara nyingi hata moyo wake kukosa amani. Hii ni sawa kabisa kwamba ilifika wakati ambapo Petro mtumishi wa Mungu alishindwa kusamehe,maana hajui asemehe mara ngapi kwa siku. Lakini kwa kusaidiwa na Bwana akafundishwa jinsi ipasavyo kuenenda katika eneo hili,Bwana kwa Roho wake akamsaidia.Na ndivyo ilivyo hata kwako,huwezi mambo haya wewe mwenyewe,bali unamuhitaji sana Roho mtakatifu akusaidie,muendee Yeye na kuomba msaada,kwanza akuondolee uchungu ulio ndani yako,naye atakusaidia tu.
02. Ukubali kushuka hata kujifanya mjinga ikiwezekana
Hivi unajua ili uweze kusamehe aliyekukosa ni wewe ndiwe unayepaswa kushuka! Lakini ukisubiri aliyekukosa ndie ashuke na kuja kwako,Je asipokuja utaendelea kumshikilia / kutomsamehe? Mwisho wake ni nini? Unaweza ukajifanya mjinga tu,ili umuokoe aliyekukosa lakini na wewe pia uweze kukubalika mbele za Mungu. Hapa itakulazimu ulipe gharama ya kunyenyekea,na ndicho kitu wanachoshindwa wengi. Lakini wewe usishindwe na hili!!#
03. Sihi / omba pendo la Mungu likukamate,uwe na upendo juu yake / yao.
Hivi unajua kwamba Yesu hakuhesabu makosa yako? Bali aliona upendo wa Mungu juu yako ingawa ulikuwa hufai na hata sasa inawezekana hufai hata sasa lakini bado kuna pendo linalokuhurumia tu. Ebu fikiria ikiwa mwanao amekukosa katika eneo fulani,je hutamsamehe ikiwa ni mwano wa kuzaa kabisa? Ikiwa utaweza kumsamehe,unajua ni kwa nini umefanikiwa kumsamehe? Jibu ni jepesi tu,ni kwamba ni kwa sababu ndani yako kuna pendo,ambapo hukuangalia kosa bali umemuona ni mtoto kakosea tu,na ndivyo ikupasavyo kumsamehe ndugu,mwenzi wa ndoa na yeyote yule. Inawezekana!
Hivi,jiulize ni madhara gani atakayokuwa nayo mtu yule asiyekuwa na moyo huu?
  1. Magonjwa yanaweza yakamuandama- kwa nini? Ni hivi,ukishindwa kusamehe unautesa moyo wako kiasi kwamba mwili hudhoofu,na hapo ndipo kwenye chanzo cha kuvamiwa na magonjwa.
  2. Kutawaliwa na hasira kali,itakayokupelekea kupata hasara maana “hasira ni hasara”
  3. Vifungo vya mapepo – kumbuka;moyo ukikamatwa na uchungu hufungua mlango wa mapepo na vifungo kukukamata.
  4. Kukonda au kunenepa sana ( najua utacheka na kuona kana kwamba hii sio,lakini ndivyo ilivyo) ebu angalia asiyeweza kusamehe katika maisha yake,hukamatwa na “msongo wa mawazo”hasa amuonapo mkosa wake. Hivyo kwa sababu hiyo anaweza akakonda sana,au anaweza kutafuta kujifariji kwa kula sana akidhani ndiyo dawa yenyewe,kumbe sio dawa ni Yesu.

No comments