MKE MWEMA
Mithali 31
1 Maneno ya mfalme Lemueli; mausia aliyofundishwa na mama yake.
2 Ni nini, mwanangu? Tena ni nini, mwana wa tumbo langu? Tena, ni nini mwana wa nadhiri zangu?
3 Usiwape wanawake nguvu zako; Wala moyo wako usiwape wale wawaharibuo wafalme.
4 Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?
5 Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.
6 Mpe kileo yeye aliye karibu na kupotea; Kampe divai yeye aliye na uchungu nafsini.
7 Anywe akausahau umaskini wake; Asiikumbuke tena taabu yake.
8 Fumbua kinywa chako kwa ajili yake aliye bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke yao;
9 Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; Uwapatie maskini na wahitaji haki yao.
10 Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani.
11 Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.
12 Humtendea mema wala si mabaya, Siku zote za maisha yake.
13 Hutafuta sufu na kitani; Hufanya kazi yake ya mikono kwa moyo.
14 Afanana na merikebu za biashara; Huleta chakula chake kutoka mbali.
15 Tena huamka, kabla haujaisha usiku; Huwapa watu wa nyumbani mwake chakula; Na wajakazi wake sehemu zao.
16 Huangalia shamba, akalinunua; Kwa mapato ya mikono yake hupanda mizabibu.
17 Hujifunga nguvu viunoni kama mshipi; Hutia mikono yake nguvu.
18 Huona kama bidhaa yake ina faida; Taa yake haizimiki usiku.
19 Hutia mikono yake katika kusokota; Na mikono yake huishika pia.
20 Huwakunjulia maskini mikono yake; Naam, huwanyoshea wahitaji mikono yake.
21 Hawahofii theluji watu wa nyumbani mwake; Maana wote wa nyumbani mwake huvikwa nguo nyekundu.
22 Hujifanyia mazulia ya urembo; Mavazi yake ni kitani safi na urujuani.
23 Mume wake hujulikana malangoni; Aketipo pamoja na wazee wa nchi.
24 Hufanya nguo za kitani na kuziuza; Huwapa wafanya biashara mishipi.
25 Nguvu na hadhi ndiyo mavazi yake; Anaucheka wakati ujao.
26 Hufumbua kinywa chake kwa hekima, Na sheria ya wema i katika ulimi wake.
27 Huangalia sana njia za watu wa nyumbani mwake; Wala hali chakula cha uvivu.
28 Wanawe huondoka na kumwita heri; Mumewe naye humsifu, na kusema,
29 Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote.
30 Upendeleo hudanganya, na uzuri ni ubatili; Bali mwanamke amchaye Bwana, ndiye atakayesifiwa.
31 Mpe mapato ya mikono yake, Na matendo yake yamsifu malangoni
Na mwinjilisiti;PROCESIUS P
No comments