VIJANA MISIYACHOCHEE MAPENZI HATA YATAKAPOONA VEMA YENYEWE

Na: Procesius prosper
c
Shalom, leo katika ukurasa huu wa maswali na majibu nataka kujibu swali kuhusu mwenendo wa vijana wakati wa uchumba ambalo limekuwa likiulizwa na wasomaji mbalimbali wa blogu hii kwa namna tofauti.
Swali: Bwana Yesu asifiwe Sanga, naomba kuuliza, je mimi na mchumba wangu kufanya michezo ya mapenzi bila kufanya tendo la ndoa ni dhambi? Mfano; kumbusu, kushikana shikana mwilini, kutekenyana, kunyonyana ndimi na yale yanayofanana na hayo? ni mimi James (James siyo jina halisi la aliyeuliza swali). Naam licha ya swali la James wapo wasomaji ambao wamekuwa wakiuliza je sisi kama wachumba kuitana honey, dear, sweetheart, baby, wife, husband nk, ni makosa au dhambi?
Wapenzi imenilazimu kujibu swali hili ili kuwasaidia vijana wengi kwa kuzingatia mitazamo yao na uharibifu wa jambo hili kwao. Binafsi nimekutana na baadhi ya vijana ambao baadhi wamehalalisha suala la michezo ya mapenzi wakati wa uchumba. Nakumbuka kijana mmoja aliniambia michezo ya mapenzi kwa wachumba sio dhambi na mwingine (binti) akaniambia leo nimekutana na mchumba wangu tukanyonyana ndimi zetu kwa zaidi ya dakika tatu, wala sioni shida yeyote, hapa nazungumzia wale waliokoka na si wasiokoka na ujumbe huu ni rasmi kwa vijana/wachumba waliokoka.
c
Ili kujibu swali husika niruhusu nikupitishe kwenye mistari kadhaa ndani ya Biblia ambayo itatusaidia kujua ukweli. Biblia katika 1Wathesalonike 4:4-7 inasema ‘kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso’. Tunatakiwa kuiweza miili yetu kwa sababu nia ya mwili ni mauti na kamwe mwili hauwezi kumpendeza Mungu.
Mwili wa mtu unaweza kuathiri roho/moyo wake na hivyo maamuzi yake pale anaporuhusu mazingira ambayo yataamsha tamaa na kuzaa matendo ya mwili. Hivyo basi ili kuuweza mwili wako sharti ujifunze kuuweza kwa  kuuzuia kufanya, kuona, kusikia, kusoma, kugusa nk au kwa kifupi kutokuuruhusu kufanya chochote ambacho kitaamsha tamaa ya mwili na hivyo kukukosesha. Hii itakusaidia uishi maisha ambayo yatamletea Mungu heshima na utukufu, maana hakutuitia uchafu.
Kwenye 1 Wakorintho 6:18-20 imeandikwa Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa MWILI WENU NI HEKALU LA ROHO MTAKATIFU ALIYE NDANI YENU, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si MALI yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu’. Kama Biblia imesema ikimbieni zinaa, je huoni kwamba kufanya michezo ya mapenzi ni kuikimbilia au kuifuata zinaa?.
b
Hata kama ninyi ni wachumba, je ni sahihi kwako utoke kushikana shikana na mchumba wako au kunyonyana ndimi, halafu kesho yake upande madhabahuni kuhudumu kwa uimbaji, neno nk, je unaelewa uzito wa sentensi kwamba mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu? Huenda iwe ulishamzimisha Roho Mtakatifu ndani yako lakini kama yu hai, naamini wakati au baada ya kitendo husika utasikia hukumu kama ishara ya kukujulisha ulichofanya siyo sahihi.
Katika 1 Yohana 2:16 imeandikwa ‘Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia’ na tena imeandikwa ‘Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu’ (Wakolosai 3:5-6) na pia katika Warumi 13:14 imeandikwa Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake’.
Ile kusema ‘vifisheni viungo vyenu’ ana maana usiruhusu mwili wako kupitia tamaa zake ukutawale, hivyo angamiza (fisha) kila aina ya uchafu (matendo ya mwili). Ndugu, usijidanganyike, kinachomuongoza mtu kufanya michezo ya mapenzi ni Shetani kupitia tamaa ya mwili na tamaa ya macho. Tamaa ndiyo inayoamsha shauku ya kufanya michezo husika ambapo itakuambia  huyu ndio mke au mmeo mtarajiwa kuna shida gani ukiwa naye karibu ili kumjua zaidi.
2
Kumbuka nia ya mwili ni mauti na wala hauwezi kumpendeza Mungu, daima mwili utakuongoza kufanya mambo ambayo ni kinyume na Mungu. Hapo ndipo bila kujua kwamba mmeshavamiwa na mapepo taratibu mtaanza kushikana, kutukenyana na mawazo mabaya yatakuja na kukuambia  mbusu shingo yake, masikio, shika matiti, makalio, chunguza mapaja yake nk. Naam kadri mnavyofanya hayo ndivyo na joto la anguko linavyopanda na mwisho wake mnafanya tendo halisi la ndoa.
Biblia katika Wimbo Ulio Bora 3:5 inasema ‘Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, MSIYACHOCHEE MAPENZI, WALA KUYAAMSHA, Hata yatakapoona vema yenyewe’Je nini maana kuyachoochea mapenzi? –  Kuyachochea mapenzi ni kufanya kitendo au jambo lolote linalopelekea kuleta uhitaji au kuamsha shauku ya kufanya tendo la ndoa. Lengo la vitendo husika ni kuamsha shauku ya kufanya tendo la ndoa na hii ina maana vitendo husika (foreplay) ni maalum kwa wanandoa tu na si vinginevyo.
Michezo ya mapenzi kwa wanandoa iko ya namna nyingi lakini inaweza kuwa pamoja na kushikana shikana mwilini, kutekenyana, kumbusa mwenza, kunyonyana ndimi, kuvaa aina fulani ya mavazi wawapo nyumbani kwao au chumbani, kuandikiana jumbe za mapenzi au kupeana maneno yenye kuziandaa fikra za mwenza kwa tendo husika nk. Ndio ni maalum kwao kwani ni sehemu ya maandalizi kabla ya kushiriki tendo la ndoa ambapo huleta hisia zao pamoja na kuamsha shauku ya kila mmoja (Wimbo ulio Bora 1:9-16, 4:10-11).
e
Sasa jiulize, biashara ya kushikana matiti, makalio, kifua, kutekenyana au kunyonyana ndimi wakati ninyi si wanandoa hauoni kwamba ni kuuwasha mwili na tamaa zake mbaya hata mkavunjiana heshima ninyi wenyewe na kulichafua hekalu la Kristo. Kitu chochote ambacho ukifanya kinafungua mlango wa tamaa ya mwili au tamaa ya macho uwe na uhakika kinalenga kukutoa kwa Mungu na hivyo kimetoka kwa Shetani.
 Jambo wasilolijua wachumba wengi ni kwamba kitendo cha kutembeleana wao pekee na kuwa kwenye mazingira hatarishi mfano nyumbani, gesti nk kwa hoja ya kutafuta utulivu ili kubadilishana mawazo, katika ulimwengu wa roho Shetani hutumia mazingira hayo kuhakikisha hawatoki salama. Naam hata kama siku hiyo hawatafanya tendo halsi la ndoa wakaishia kucheza uwe na uhakika fikra za kipepo ambazo zimepandwa ndani ya kila mmoja, kama hawataziangusha, zitahakikisha siku za usoni zinawaangusha wao dhambini. Wachumba wengi wameanguka kwa jinsi hiyo hivyo wewe jizuie kabisa kukutana na mwenza wako mazingira yatakayomualika Shetani kuwatembelea na kuwakosesha.
6
Ndiyo maana Paulo anaagiza akisema ‘Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili’(Wagalatia 5:16). Ndio ni kwa kuenenda kwa roho ndivyo mwamini anavyoweza kutouangalia mwili hata kuziwasha tamaa zake. Sheria au utaratibu wa Roho Mtakatifu utakuongoza na kukuonyesha njia sahihi ya kuiendea hata katika kipindi cha uchumba wenu (asomaye na afahamu).
Pia tambua kwamba uchumba sio ndoa, ukiwauliza wanandoa wengi leo watakuambia mume au mke aliye naye sasa si yule ambaye alikuwa mchumba wake wa kwanza. Ukikosea ukamruhusu mchumba wako alale na wewe kipindi cha uchumba ukidhani ndio atakupenda umekosea maana biblia inasema utapata jeraha na kuvunjiwa heshima tena fedheha yako haitafutika (Mithali 6:32-33). Hii ni moja ya sababu ya baadhi ya mabinti waliokuwa kwenye uchumba kuachwa na kuishia pabaya maana sio wote walioweza kuyakabili maumivu ya kuachwa.
1
Naamini umeshawahi kuwasikia vijana wakisema nilimpenda sana dada fulani na nilitaka kumuoa ila baada ya kulala naye nimeona ni wa kawaida sana au ana kasoro fulani hivyo siwezi kumuoa. Ukweli ni kwamba unaweza ukaona hata hiyo shida huyo dada hana ila kwa sababu alifungua mlango wa uharibifu Shetani amepitia hapo kupandikiza roho ya chuki/uharibifu ndani ya kijana dhidi ya binti hata kijana hataki kuoa tena.
t
Sasa ikiwa uchumba sio ndoa, kwa nini ufanye mambo ya wanandoa wakati wewe si mwanandoa. Je kwa nini kumruhusu mtu asiye mumeo au mkeo kunyonya ulimi wako au kuchezea mwili wako kwa kushika makalio, matiti, kutazama tupu yako nk, je akikuacha wakati tayari anaujua mwili wako vizuri na huenda ulishalala nye huoni ni fedheha? Je umesahahu kwamba mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu?, kwa nini usimtunzie Mungu heshima yake hata utakapopata mwenza wako halali nanyi mkawa huru katika Bwana?
Binafsi nimekutana na kuzungumza na wachumba wengi ambao walifanya makosa husika. Nimejifunza na kuthibitisha kwamba wengi hawakuishia kucheza tu bali zaidi walifanya tendo la ndoa kabisa. Baadhi ya wachumba michezo hiyo iliwasha tamaa isiyo ya kawaida ndani yao na huo ndio ukawa mwanzo wa utumwa wa uasherati/zinaa, kufanya ngono ndotoni, kujipiga punyeto nk. Hakika michezo ya mapenzi haijawahi kuwaacha wachumba salama kiroho na kimwili kwa sababu wanaitumia kinyume na neno la Mungu na hivyo Shetani anapata uhalali wa kuwaharibu.
Pale walipofikiri ni michezo ya kawaida Shetani alitumia michezo husika kuwanasa na kupandikiza ndani yao roho chafu kupitia mapepo yanayokaa kwenye macho, midomo, mate, mapaja nk ambayo huwaingia na kuathiri maisha yao kwa kuanzisha tabia zisizo za kawaida. Tambua si kila mwanaume au mwanamke anayekuja kwako kukuchumbia ametokana na Mungu, wengine ni wajumbe maalum wa yule mwovu.
r
Pale wachumba wanapofikiri michezo hiyo ni halali tena wako salama, hawajui nyuma yake kuna jeshi la mapepo linaloongoza fikra na maamuzi yao ili kufanya michezo husika. Ndio wengi wao hawakujua kwamba hawako salama wala kutafuta kutengeneza hadi pale walipoona matokeo ya michezo hiyo kwa macho ya damu na nyama. Baadhi yao waligundua kwamba michezo hiyo ni hatari pale walipojikuta wamezini kabisa tena si mara moja. Wengine kuzini haikuwa shida kwao hadi pale binti aliposhika mimba, naam kwa wengine mimba haikuwa shida au sababu ya kutengeneza bali wakaona bora watoe mimba au walazimishe ndoa ifungwe haraka, naam hawa wote tunao makanisani.
Hapo ndipo unajiuliza maswali magumu kwamba ni nani aliyewaloga? ni Mungu yupi wanamwabudu? Ni Biblia gani wanasoma? Je Roho Mtakatifu yu hai ndani yao au walishamzimisha? Hoja ya msingi inayopelekea maswali hayo si kuanguka bali zaidi, kwa nini baada ya kuanguka hawakuona kuwa wamemtenda dhambi wakatengeneza hadi walipoona matokeo ya michezo ya mapenzi kupitia zinaa, mimba au hadi pale Mtumishi alipofunuliwa juu ya dhambi yao ndio nao walishtuka? Hii ina maana isingekuwa mimba au watumishi waliokaa vizuri na Mungu kufunuliwa uovu husika, wachumba hao wangeendelea hivyo hadi kufunga ndoa.
5
Kumbuka Biblia inasema msidanganyike, mazungumzo mbaya huharibu tabia njema. Hii ni kwa sababu ndani ya mazungumzo mabaya kuna kitu huachiliwa ambacho kinaathiri tabia ya mtu. Sasa endapo mazungumzo mabaya huharibu tabia njema, je si zaidi michezo ya mapenzi ambayo wahusika hawaifanyi hadharani bali kwenye mazingira ya usiri? Je si kwamba hata dhamiri zao zinawashuhudia kwamba jambo hilo si sahihi?
Hivyo basi sio sahihi kwa wachumba kufanya michezo ya mapenzi kwa sababu mosi neno la Mungu limekataza na pili michezo ya mapenzi ni maalum kwa wanandoa na si vinginevyo. Pale ambapo wachumba watafanya michezo husika itapelekea kuamsha tamaa ya mwili ambayo itazaa dhambi nyinginezo na hivyo kuharibu mahusiano ya mtu na Mungu wake.
 Kumbuka mahusiano hayo ni ya muhimu sana kwa pande zote ili kuruhusu mawasiliano kati yao, mahusiano yakiharibika, mawasiliano yatakatika na mawasiliano yakikatika hakutakuwa na mafunuo ya Mungu na pasipokuwa na mafunuo mwenye kuathirika zaidi ni mwanadamu maana ataishia pabaya  (asomaye na afahamu).  
8
Naam, nami kwa neema ya Mungu niliyopewa, neema ambayo ilitusaidia mimi na mke wangu tusianguke dhambini katika kipindi husika licha ya changamoto nyingi za ujana na hila za Shetani, kwa ujasiri katika Kristo Yesu nawaambia, msidanganyike, michezo ya mapenzi ni mlango mkubwa wa uharibifu ambao Shetani anautumia kuharibu maisha (future) ya vijana wengi sana na kuwaondoa kwenye kusudi la Mungu bila wao kujua, hivyo jihadhari, usiyachochee mapenzi kwa namna yoyote ile hata muda wake utakapotimia.
 Utukufu na heshima vina wewe Yesu, wastahili BWANA wangu