MAISHA BAADA YA MUUJIZA WAKO.
Bwana Yesu asifiwe…
Kulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa haondoki kanisani akiomba na kufunga. Alikuwa akihitaji kupata mtoto maana ameishi ndani ya ndoa muda mlefu hivi bila kupata mtoto. Akiwa amekaza katika maombi mara akajibiwa maombi yake. Akafanikiwa kupata mtoto,akafurahi sana. Lakini hali yake ya kimaombi ikashuka,hakuwa na kiu tena ya kungangana katika maombi kwa kuwa alichokuwa akikihitaji amekwisha kupata kwa maana yeye alifikiri ya kwamba tarajio la kupata mtoto ndio kila kitu.
Kilichokosekana kwa mwanamke huyu ni namna ya kuukumbatia ule muujiza,hakujua kwamba kuna maisha mengine baada ya muujiza. Na ndivyo watu wengi wafanyavyo leo. Mara nyingi watu wanamuacha Mungu wakishatendewa muujiza,ni kama vile wanabweteka kwa sababu ya muujiza mmoja. Angalia mfano huu tena; kuna watu wanaomba Mungu awape mali, hali wanaonekana kabisa kwamba wakipewa mali watamsahau Mungu. Utakuta mtu anaomba apate pesa za kutosha alafu akisema``Mungu ukinipa pesa nzuri ya kutosha,nitakutumikia sana,nitajitoa kwa kila kitu. Nitawasaidia wasiojiweza,nitatoa zaka na kulipa michango ya ujenzi kanisa…nk”
Lakini ngoja sasa apate hizo pesa,we! Ndio kwanza utamsikia akisema“mchungaji,nipo bize jamani,sasa naelekea kariakoo…nina duka langu kule,….kweli ninajua kwamba leo ni ibada lakini hata Mungu mwenyewe anajua kwamba mimi nipo bize,ngoja nikimaliza biashara nitakuja…nk” umeona,yaani mtu wa namna hii anathubutu hata kumtaja Mungu katika ubize wake!Watu wa namna hii wameiacha imani kwa sababu ya kupata walichokuwa wakikihitaji. Kwa sababu hitaji lao si Mungu bali ni mambo ya kupita tu.
Tujifunze kwa mtu mmoja aliyetendewa muujiza kisha tuangalie maisha yake baada ya huo muujiza. Yupo mtu mmoja aliyekuwa kiwete tangu tumboni mwa mamaye. Mtu huyu alikuwa akichukuliwa na watu na kuwekwa penye mlango wa hekalu uitwao mzuri kwa ajili ya kuomba sadaka kwa wale waliokuwa wakiingia na kutoka hekaluni. Mtu huyu alipokutana na Petro na Yohana huku akitaraji kupata kitu kutoka kwao, Lakini Petro akasema, “ Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.” Matendo 3:6-7
Muujiza ukafanyika kwa huyu mtu,akasimama na akaenda. Watu wote wakapigwa na butwaa kwa maana hawakujua kwamba Mungu anaweza kufanya hivyo kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Muujiza huu ulikuwa maalumu kwa sababu kwanza mtu huyo alikuwa kiwete toka tumbuni mwa mamae si kana kwamba labda alizaliwa akiwa mzima,lah! Bali alikuwa kiwete,Bwana Mungu alikuwa anawafundisha kwamba ni Yeye tu ambaye Mungu wa kweli asiyeshindwa kitu. Angalia kilichofuata kwa mtu huyu baada ya kupokea muujiza wake,;Biblia inasema;
“ Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu Mungu.” Matendo 3:8
Tunajifunza nini kwa huyu aliyekuwa kiwete baada ya kupokea muujiza?
Alikaza kwa Mungu akimsifu na kuruka ruka hekaluni. Maisha yako baada ya kutendewa na Bwana yanatakiwa yatolewe kwa Mungu,umuone Mungu ndie katenda. Maana biblia haituambii kwamba yule aliyekuwa kiwete alikwenda nyumbani kwa akina Petro,bali tunaambiwa aliingia hekaluni akimsifu Mungu;kwa lugha nyepesi aligundua kwamba ni Mungu ndie aliyetenda wala si mwanadamu wa kawaida.Yakupasa kujua kwamba ni namna gani utamuhimidi Bwana baada ya kujibiwa maombi yako. Ni watu wachache sana wanaokaza kwa Mungu baada ya kutendewa muujiza.
Swali la kujiuliza;
Je ulipotendewa na Bwana ulishuhudia matendo ya Bwana?
Mtu huyu anatufundisha kwamba,ikiwa umetendewa na Bwana yakupasa ushuhudie uweza wa Bwana kwa wengine kusudi kushuhudia kwako kuwajenge kiimani wengine. Kwa maana wapo watu wasioamini mpaka waone kwa macho. Ni mara ngapi unashuhudia miujiza yako hadharani?
Angalia matokeo ya ushuhudiaji kwa mtu huyo aliyekuwa kiwete;
- Akina Petro walipata mkutano wa bure usiokuwa na gharama (. Kwa sababu mkutano wa leo una gharama sana katika kila kitu,lakini haikuwa hivyo kwa akina Petro.) Yule ndugu aliposhuhudia akaamsha hisia za watu,watu wakakusanyika pasipo kuombwa na Petro akawahubiria. Lakini haya yote yamekuja kwa sababu ya mtu mmoja aliyeshuhudia baada ya muujiza. Hata leo,ukishuhudia muujiza wako,utasababisha kuwafanya watu wakusikilize pamoja hata kama walikuwa hawataki,bali ujumbe utawafikia tu.
- Kuokoka kunaletwa na nguvu ya ushuhudiaji.-Tunaona tokeo hili likifanyika,watu wapata elfu tano tena hao ni wanaume bila kuhesabu wanawake na watoto. wakampa Yesu maisha yao( Matendo 4:4). Chanzo kikubwa cha watu kukata shauri ni baada ya kusikia habari za Yesu Kristo,hata leo tunaokoka kwa sababu tumesikia habari zake Yesu,tukaziamini. Mtu mmoja akishuhudia mtaani au mahali popote alipo,ujue ana nguvu ya kuvuna roho nyingi zilizopotea.
Kumbuka; muujiza wako usiwe chanzo cha kumuacha Mungu,bali uwe chanzo cha kumpenda zaidi Bwana Mungu wako ili utendewe zaidi. Pale upatapo shuhuda,muombe Roho mtakatifu akusaidie uweze kushuhudia kwa watu wote ili umpe Mungu utukufu.
No comments