NJIA SABA(7) ZA KUPIGANA VITA YA KIROHO KWA MAOMBI(Sehemu ya pili)
Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu.
Namshukuru MUNGU sasa naenda kumalizia somo langu ambalo liligusa wengi maana wengi walinijulisha kwa meseji na whatsap wakiulizia mwendelezo wake, hiyo ilinipa nguvu sana kwamba wapo watu wenye kiu na njaa ya haki, yaani wenye kiu ya kujifunza Neno la kweli la MUNGU.
Mathayo 5:6 ''Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa.''
Nilisema vitu vingi katika somo hilo ambavyo naamini vilikusaidia sana katika kupigana vita ya kiroho.
Kuna njia kadhaa Biblia inazitaja kama njia za kupigana vita ya kiroho kwa maombi. Husika nazo itakusaidia.
Sasa naendelea njia ya pili na kuendelea.
2. Kufunga na kufungua.
Mathayo 16:19 ''Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.''
Hii ni njia yenye vipengele viwili tofauti lakini kila kipengele kinamhitaji mteule wa KRISTO.
Kufunga maana yake kukataa jambo lisitokee.
Kufunga ni kuzuia jambo la kishetani ambalo lilipangwa likupate, lakini kwa maombi yako ya kulizuia hakika jambo hilo halitakupata.
Unaweza ukazuia ajali kwa maombi yako, unaweza ukazuia ugonjwa, unaweza ukazuia kuonewa, unaweza ukazuia kuteswa na wachawi, unaweza ukazuia kutokuzaa, unaweza ukazuia kila kazi ya shetani katika maisha yako. Ni Mamlaka hiyo MUNGU amekupa kama Mteule wake ili ukizuia vitu katika ulimwengu wa roho hakika vinazuiliwa.
Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.''
Kipengele cha pili ni kufungua.
Hiyo maana yake unaruhusu kilicho cha MUNGU kitokee.
Unaruhusu kilicho haki yako ambacho kilizuiliwa kipepo sasa kitokee kupitia maombi yako ya kufunga kazi za shetani na kufungulia baraka zako.
Katika njia hii ya kufunga na kufungua ni muhimu sana kuwa mtu unayeongozwa na ROHO MTAKATIFU ndipo utashinda kwa urahisi.
Kumbuka sio vitu vyote unaweza kufunga na sio kila kitu unaweza kufungua. Maombi ni somo pana sana na maombi sahihi ni yale ambayo ROHO MTAKATIFU anakuongoza tu.
Kazi ya ROHO MTAKATIFU ni kutuongoza katika kweli ya MUNGU hivyo hata katika maombi yako ya kufunga kazi za shetani na kufungulia baraka zako zilizokuwa zimeshikiliwa kipepo na mawakala wa shetani hakika unamuhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili akujulishe ni nini cha Kufunga kwa maombi na ni nini cha Kufungua kwa maombi.
Ukikataa ushauri na maongozo ya ROHO MTAKATIFU huwezi kuwa sahihi hata siku moja.
Zaburi 32:8 '' Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''
Mteule wa MUNGU una mamlaka kuu sana MUNGU amekupa kwa sababu umekubali kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako, lakini mamlaka ya kimaombi ya kufunga mambo ya giza na kufungua mambo ya baraka unahitaji sana sana ROHO MTAKATIFU akufundishe na kukujulisha.
Ndugu unayo mamlaka kubwa sana ambayo wasio na YESU hawana, wasio na ROHO MTAKATIFU hawana lakini unahitaji sana kumwambia ROHO MTAKATIFU akusaidie na kukujulisha ni vitu gani vya kufunga na ni vipi vya kufungua.
3. Kuziondoa nguvu za giza ndani ya mtu.
Marko 16:17-18 '' Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu WATATOA PEPO; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.''
Maandiko haya yana vitu vingi lakini kwenye somo langu nahusika na kanuni/Njia za kiroho za kupigana vita ya kiroho.
Njia hii inaitwa kutoa nje nguvu za giza ndio maana Biblia inasema ''Watatoa mapepo''
Mapepo ni nguvu za giza ambazo zinaweza zikawekwa na mawakala wa shetani popote.
Wengi sana wanateswa na majini ambayo ndiyo hayo hayo mapepo.
Unaweza ukateswa na ugonjwa mbaya sana na ambayo huwa unaondoka na kurudi kumbe ulirushiwa jini likajigeuza ugonjwa usiopona na ugongwa huo unakutesa.
Kuna ambao hadi walikufa kwa kuteswa na magonjwa ya ajabu huku hawajui kama ni majini walirushiwa yakajigeuza ugonjwa ndani ya miili yao na magonjwa hayo yanawatesa na wengine magonjwa mengine hata wakienda hospitalini vipimo havionyeshi kama wanaumwa, lakini wao wanaumwa sana sana.
Hata biashara yako inaweza ikarushiwa majini na wachawi wanaokusakama.
Ufahamu wako unaweza ukatupiwa mapepo kiasi kwamba huwa unalitumikia kusudi la shetani na sio la MUNGU.
Mapepo kama nguvu za giza zinaweza zikatesa ndoa, ukoo, familia au mwili wako.
Neema ya MUNGU ni ya ajabu sana sana maana kwa waliookoka haswa MUNGU ametupa Mamlaka na uwezo wa kuwatoa nje majini wote na kila nguvu za giza ili watoke katika miili yetu na maisha yetu.
Bwana YESU alisema kwamba moja ya kazi za wateule wake ni kuzitupa nje kazi za shetani ziitwazo mapepo/majini.
Ni kazi ya mteule wa KRISTO kuyatoa nje ya mwili au familia au ukoo au biashara mapepo yote yaliyotumwa.
Njia hii ya kutoa nguvu za giza ili ziondoke kwako umepewa na MUNGU, Itumie kanuni hii vyema na MUNGU Baba atakushindia katika jina la YESU KRISTO.
Mfano wa wateule waliotoa mapepo kama alivyoagiza Bwana YESU ni huyu mtume Paulo.
Matendo 16:18 ''Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la YESU KRISTO, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile. ''
YESU ni yule yule na hajawahi kupunguza viwango vya mamlaka yake kwa wateule wake,
Ndugu hakikisha kanuni hii ya kutoa nje nguvu za giza unaitumia katika maombi yako, ni kanuni muhimu sana kwa muombaji makini.
Mapepo sio lazima yakae katika mwili wako tu, yanaweza yakakaa kwa mke wako au mume wako, yanaweza yakakaa kwa watoto wako au marafiki zako, mapepo yanaweza yakakaa kwenye kundi lenu na yanaweza yakakaa kwenye biashara yako au kazi yako.
Ni rahisi tu, umepewa mamlaka ya kuwatupa nje na hawana uwezo wa kukataa kutoka.
Hakikisha tu unaishi maisha matakatifu na unaliishi Neno la MUNGU.
Kwa sababu ni kumtupa nje adui basi ni muhimu sana kujua kwamba hutakiwi kumbembeleza adui huyo bali ni kukemea kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO.
4. Kushindana.
Waefeso 6:11-13 ''Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
Tunashindana kimaombi na tunashinda.
Tunashindana na viumbe wasioonekana lakini tunawashinda na kuwangamiza.
Ni Mamlaka tumepewa na ni ushindi kwetu ni lazima.
Ni muhimu sana kuomba maombi ya kushindana na adui ili umshinde.
Kumbuka adui hakuogopi wewe ila anamuongopa YESU KRISTO Mwokozi wako.
Adui anamuogopa ROHO MTAKATIFU aliye ndani yako.
Unahitaji kuwa muombaji sana ili uwashinde maadui zako kiroho.
Kiufunuo unaweza kujikuta hata unaomba maombi ya kufunga ili kuwashinda maadui zako.
Mawakala hao wa shetani wanajua kabisa kwamba wewe ukikaa katika nafasi yako ya maombi hakika unawashinda na kuwadhuru sana, ndio maana moja ya kazi ambazo shetani anazifanya kwako ili akufunge zaidi basi ni kuhakikisha hujifunzi Neno la MUNGU la kukusaidia na huombi.
Lakini kwa wanaojitambua hakika uko ushindi mkuu kutoka kwa MUNGU kwa wewe kuomba maombi ya kuwapiga adui zako ili wakimbie.
Shetani na watoto wake hawana jinsi wakisikia jina la YESU KRISTO, Ni lazima wakimbie hakika. Ndugu hakikisha unaitumia mamlaka ya KRISTO iliyo ndani yako kuwashinda maadui zako.
Biblia inasema ''Kushindana kwetu sio juu ya damu na nyama'' maana yake kumbe tunapaswa kushindana na mawakala wa shetani.
Usiposhindana nao watakuonea sana maana hawatakutana na vita wakikuvamia.
Ndugu itumie kanuni hii ya kushindana nao ili uwashinde.
Huwezi ukawa na jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Nguvu za ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU harafu adui ashindwe kukukimbia, haiwezekani.
Unahitaji kuomba maombi ya kuwashindana maadui zako, hiyo ni kanuni ya kimaombi na njia ya kimaombi inayokuhitaji wewe muombaji.
Msaada wa MUNGU huwa ni mkubwa sana kwa mtu anayejua kupigana vita vya kiroho vya kushindana na mawakala wa shetani.
Yeremia 1;19 '' Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe. ''
5. Kupinga.
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. ''
Hii kanuni muhimu sana yaani kimaombi unapinga kila kazi ya shetani na hakika haitafanikiwa kazi hiyo ya giza.
Kumtii MUNGU ndio kumpinga shetani.
Tunahitaji kumpinga shetani katika mambo yake yote, ni kanuni ya wateule wa MUNGU.
Kipengele hiki kina maana ya kumwingilia shetani katika kazi zake na kumzuia kuendelea kufanya kazi hizo, hiyo ni mamlaka ya mteule wa MUNGU.
Tunampingaje Shetani?
1.Tunampinga shetani kwa maombi ya kumpinga.
2. Tunampinga kwa kukataa kufuata kazi zake na matendo yake.
3. Tunampinga shetani kwa sisi kulitii Neno la MUNGU.
4. Tunampinga shetani kwa sisi kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
5. Tunampinga shetani kwa Neno la MUNGU.
1 Petro 5:8-9 ''Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. ''
Ndugu, ni kazi yako na jukumu lako kumpinga shetani.
Kumpinga shetani ni kanuni ya kimaombi iliyo muhimu sana.
Kumpinga shetani ni kumzuia kuendelea kukunyanyasa na kukuonea.
Kumpinga shetani ni kumkataza kuingilia ndoa yako, uchumi wako, uchumba wako, au akili yako.
Kwa maombi hakika unaweza kuwapinga ,mawakala wa shetani na wakakimbia hakika maana wanajua kwamba yeye shetani hana nguvu hata moja kwa aliyeko ndani yetu yaani ROHO wa MUNGU wetu.
1 Yohana 4:4 ''Ninyi, watoto wadogo(Wateule wa KRISTO), mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda(Mawakala wa shetani), kwa sababu yeye aliye ndani yenu(ROHO MTAKATIFU) ni mkuu kuliko yeye(Shetani) aliye katika dunia.''
6. Angusha.
2 Kor 10:3-5 '' Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya MUNGU; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii KRISTO; ''
Kanuni nyingi muhimu ya kimaombi ni kuteka fikra ili zipate kumtii YESU KRISTO.
Ni kanuni ambayo kanisa la MUNGU linaagizwa liitumie katika maombi.
Unaweza ukawa na mawazo ndani yako ya kufanya kitu fulani kumbe ni mawazo ambayo hayatokani na MUNGU, Usipojua kuyaangusha mawazo na fikra mbaya ambazo ziko kinyume na Neno la MUNGU hakika unaweza kujikuta wewe ni mtu wa kufanyia kazi wazo la shetani kila siku na mwisho wake hakuna baraka za MUNGU katika wazo lililotokana na shetani.
Hakikisha unaangusha kila fikra iliyo kinyume na Bwana YESU ndipo utapata fikra ya MUNGU.
Tiisha mawazo yako ili yawe mawazo yanayokubaliana na Neno la MUNGU.
Kuna mawazo ya kipepo mengi tu yanaweza kukukumba na hakikisha unaangusha mawazo hayo na fikra hizo zilizo kinyume na Neno la MUNGU.
Moja ya fikra ambazo inawezekana unazo na hizo fikra ni potofu sana na za kipepo ni hizi hapa.
1. Mawazo ya dhambi.
2. Mawazo ya kujilaumu.
3. Mawazo ya kujiona hufai hata kama umeshatubu na kuokoka.
4. Mwazao ya kujihukumu bila kosa
5. Mwazao ya kujidhania huwezi bila watu fulani n.k
Ni aina nyingi sana za mawazo ya kipepo ambayo mtu wa MUNGU unaweza kujikuta unafanyia kazi na kwa njia hiyo unapishana na kusudi la MUNGU.
Unahitaji sana kuitumia kanuni hii ya kimaombi ya kuangusha kila mawazo na fikrra ili zipate kumtii KRISTO na Neno lake.
Mawazo ya shetani siku zote yako kinyume na Neno la MUNGU.
Hakikisha unaangusha kila fikra na mawazo ili yapate kumtii KRISTO.
Tumia kanuni hiyo ya kimaombi ya kuangusha fikra na mawazo mabaya yote ili yasifanye kazi katika maisha yako.
7. Kung'oa, Kubomoa, Kuharibu na kuangamiza
Yeremia 1:10 ''angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. ''
Kazi ya kung'oa kazi za shetani ni kazi yako mteule.
Kazi ya kung'oa vifungo vya kipepo katika familia yako au ukoo wenu ni yako mteule kupitia maombi.
Kazi ya kubomoa madhabahu za kishetani katika maisha yako au jamii yako au ukoo wako ni yako mteule wa MUNGU.
Kuna madhabahu nyingi tu za giza ambazo unahitaji kuzibomoa katika ukoo wako, familia yako au jamii yako.
Kuna madhabahu za ulevi.
Kuna madhabahu za uzinzi na uasherati.
Kuna madhabahu za uchawi na kutegemea waganga.
Kuna madahabu za magonjwa n.k
Ziko mashabahu nyingi tu za giza na hizo inakupasa wewe kupitia maombi yako kuzibomoa ili ziondoke.
Kuna mambo yanahitaji kuharibu na kuna kuna silaha za shetani zinahitaji kuangamizwa kabisa.
Kwa sababu kuna kung'oa, kubomoa, kuharibu na kuangamiza basi mteule wa MUNGU unahitaji sana kuwa mtu wa rohoni unayeongozwa na ROHO MTAKATIFU ili ujue ni wapi pa kupomoa na ni wapi sio pa kubomoa ila ni pa kuangamiza.
Ukimtii ROHO MTAKATIFU atakusaidia kujua ni wapi wa kuharibi na ni pa kuvunja.
Nimewahi kuandaa somo kuhusu KUNG'OA, KUBOMOA, KUHARIBU NA KUANGAMIZA na huko nilifafanua sana kuhusu kipengele hiki.
Naamini kabisa sasa unajua kuzitumia Kauni hizi saba za kimaombi ili kukusaidia kumshinda shetani na jeshi lake lote la waganga, wachawi, wakuu wa giza na majini wote.
Kumbuka wewe ni salaha ya MUNGU ya ajabu sana kama utaamua kuokoka na kuomba huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Yeremia 51:20-23 '' Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake; na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke; na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida. ''
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.

1 comment: